Wacha tuseme…
Tuseme bahari liwake nyekundu,
mawimbi yapande yafurike ndoto.
Tuseme maisha yavuruge.
Tuseme macho yetu yasiachane kwa hofu.
Tuseme usiku ujitangaze mchana.
Tuseme aliyetarajiwa haji.
Tuseme maneno yamekata, yamekataa.
Tuseme mti uanguke na mtiririko wa maji
umwagike barabarani, ukivuta ujana.
Tuseme busara ya kuona mengi ufichwe
na masaibu ya mwili. Ya maisha.
Tuseme ngazi tuliyopanda nayo ivunjike,
na tuachwe tukianguka hewani, kila sekunde
tunakaribia mwisho wa tujuayo, wa tutakayo.
Tuseme mapenzi yakuondoke. Yakuzubaishe.
Tuseme wema upite njia tofauti, na uukimbize
kwa sura, kwa maneno, kwa vitendo, kwa dini.
Tuseme baridi shadidi ituzingire, mimi na wewe
kwenye ufuo wa uoga wetu. Tukikumbatiana.
Tuseme mwisho ujitangaze ghafla.
Sema tutajipata tunaamua pamoja, kimoja.
Sema dunia ni sisi, ni tujuayo, ni tuwajuao;
kwamba hushtushwi, hubabaishwi – kwamba
mikono yetu, mioyo yetu karibu, tutasakata,
tutasema yaliyo yametosha. Sema wakati ukija
wa kutafakari upana wa zilizo, walio, kuliko, vilivyo –
utatuona na kufikiria: bahati iliyoje[i].
[i] Soma The Conditional iliyoandikwa na Ada Limón. Nilivutiwa na uandishi wake na nikajipata nikitunga sentensi kwa Swahili, moja baada ya nyingine. Matokeo ni shairi hii.